Timu ya JKT Queens pamoja na Viongozi na Benchi la Ufundi wameondoka Novemba 5 mwaka huu kwenda nchini Misri kushiriki Michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa upande wa wanawake Michuano hiyo inatarajiwa kuanza rasmi Novemba 8 mwaka huu hadi Novemba 21 mwaka huu.
Katika hatua hiyo mkuu wa Tawi la Utawala JKT Brigedia Jenerali Hassan Mabena kwa niaba ya Mkuu wa JKT Meja Jenerali Rajabu Mabele, amewasindikiza wachezaji hao katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere na kuwatakia kila la heri katika michuano hiyo.
Aidha timu ya JKT Queens ndio mabingwa wa Ligi Kuu ya NBC kwa upande wa Wanawake katika msimu wa 2024/2025, lakini pia ni mabingwa wa mpira wa miguu kwa upande wa wanawake katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), ubingwa ambao umewapa tiketi ya kuwakilisha ukanda wa CECAFA katika Mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa upande wa wanawake.