Waziri wa utamaduni, Sanaa na Michezo
Mhe. Mohamed Mchengerwa Februari 15, 2022 amekutana na Balozi wa
Morocco nchini Mhe. Zakaria Elgoumiri na kufanya mazungumzo ya
kuendeleza sekta za michezo, utamaduni na Sanaa ambapo Balozi
amesisitiza serikali yake ipo tayari kushirikiana na Tanzania kwa faida
ya wananchi wa nchi hizo.
Mhe. Mchengerwa amesema Serikali ya
Tanzania na Morocco zimekuwa na uhusiano mzuri katika sekta hizo toka
muda mrefu hali ambayo imewafanya viongozi wakuu wa nchi zote kufanya
ziara na kubadilishana uzoefu wa sekta hizo.
Akiwa katika kikao
hicho ambacho aliambatana na Katibu Mkuu wa Utamaduni, Sanaa na Michezo.
Dkt, Hassan Abbasi, Mkurugenzi wa michezo nchini Yusufu Singo na Katibu
Mtendaji wa Baraza la Taifa la Michezo (BMT) Neema Msitha wamekubalina
na ujumbe wa Mhe. Balozi wa kuendelea kushirikiana kwenye sekta hizo.
Ameyataja
baadhi ya maeneo ya kipaombele ambayo yanakwenda kufanyiwa kazi kuwa ni
ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya michezo, maeneo ya tamthilia na
filamu pamoja na kushirikiana kwa pamoja kuandaa matamasha ya Sanaa na
Utamaduni.
Mhe. Mchengerwa amewakaribisha kushiriki katika
matamasha makubwa ya kihitoria ya Serengeti litakalofanyika jijini
Dodoma Machi 12,2022 na Tamasha la Kimataifa la Utamaduni na Sanaa
Bagamoyo.
Kwa upande wake Mhe. Balozi Elgoumiri amesema Serikali
ya nchi yake inafurahishwa na Sera na diplomasia ya uchumi ya Serikali
ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Rais Samia Suluhu
Hassan hivyo ipo tayari kuendelea kushirikiana na ustawi wa wananchi wa
pande zote mbili.
Ameuomba upande wa Tanzania kukamilisha andiko iliutiaji Saini ufanyike mara moja.
“Tupo
tayari kusaini andiko la kukuza ushirikiano kwenye maeneo
tuliyokubaliana wakati wowote andiko litakapokuwa tayari”. Amesisitiza
Mhe Elgoumiri