Bennett kukutana na mfalme, mrithi wa ufalme wa Bahrain

Wakati hatima ya mazungumzo ya Mkataba wa Nyuklia wa Iran na mataifa makubwa duniani ikiwa haijuilikani, Waziri Mkuu wa Israel Naftali Bennett yuko ziarani nchini Bahrain kuimarisha mahusiano baina ya nchi mbili hizo..

Baada ya kuwasili siku ya Jumatatu (Februari 14) na kulakiwa kwa hamasa kubwa mjini Manama na Waziri Mambo ya Nje wa Bahrain, Abdullatif bin Rashid Al-Zayani, hivi leo (Jumanne, Februari 15), Bennett anatazamiwa kukutana na Mfalme Hamad na pia mrithi wa kiti cha ufalme aliye pia waziri mkuu wa taifa hilo dogo, Salman bin Hamad.

Ziara hii ya Bennett ni ya sehemu ya jitihada za hivi karibuni kabisa kujikurubisha na mataifa ya Kiarabu, kufuatia kile kinachoitwa Mkataba wa Abraham uliosimamiwa na Marekani mwaka 2020, ambao unavunja makubaliano ya muda mrefu ya mataifa ya Kiarabu kutokuwa na mahusiano na Israel bila ya kwanza kuwepo kwa suluhisho la kudumu kwa mgogoro wa Israel na Palestina.

Bahrain na mshirika wake wa karibu, Umoja wa Falme za Kiarabu, zilizifuata Misri na Jordan kwenye kuanzisha mafungamano na Israel baada ya kusaini makubaliano yaliyosimamiwa na rais wa wakati huo wa Marekani, Donald Trump. Bennett aliutembelea Umoja wa Falme za Kiarabu mwezi Disemba mwaka jana.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii