Mshambulizi wa Paris Saint-Germain, raia wa Ufaransa, Ousmane Dembele, ameshinda tuzo ya Ballon d'Or 2025 usiku wa Jumatatu, akimshinda Lamine Yamal wa Barcelona (Mchezaji Bora Chipukizi). Tuzo hii ya kibinafsi inaungana na zile za Kipa Bora (Gianluigi Donnarumma) na Kocha Bora (Luis Enrique) katika kutambua msimu mzuri wa Paris Saint-Germain. Naye Aitana Bonmati ameshinda tuzo ya wanawake kwa mara ya tatu mfululizo.
Dunia ya kandanda imekutana katika sherehe ya kifahari kwenye ukumbi wa Théâtre du Châtelet jijini Paris kubaini ni nani ataibuka mshindi mpya wa tuzo hii, ambayo kwa muda mrefu ilitawaliwa na Lionel Messi na Cristiano Ronaldo.
Wawili hao walishinda Ballon d’Or mara 13 kati ya mwaka 2008 hadi 2023. Tuzo hii, inayotambulika kama heshima kubwa zaidi ya mchezaji mmoja mmoja katika soka, ilikwenda kwa kiungo wa Manchester City, Rodri, mwaka jana baada ya kuiongoza Uhispania kutwaa ubingwa wa Euro 2024.
Kwa kuwa Rodri hayupo kwenye kinyang’anyiro mwaka huu baada ya kuumizwa msimu uliopita, Dembele mwenye umri wa miaka 28 ameibuka kuwa kipenzi cha mashabiki miongoni mwa orodha ya wateule wengi kutoka mabingwa wa Ligi ya Mabingwa, PSG.
Mshambulizi wa Paris Saint-Germain, Ousmane Dembele, amemshinda nyota chipukizi wa Barcelona, Lamine Yamal, na kushinda tuzo ya Ballon d’Or ya wanaume usiku wa Jumatatu Septemba 22.
Dembele alionekana tangu mapema kuwa na nafasi kubwa zaidi baada ya msimu wa kushangaza alipopachika mabao 35, akijaza pengo lililoachwa na Kylian Mbappé aliyeondoka. Mchango wake uliisaidia PSG kushinda mataji yote ya ndani na pia kufika fainali ya Kombe la Dunia la Vilabu.
“Ilikuwa ni msimu mzuri sana na PSG. Ni heshima kubwa kuwa miongoni mwa wanaopewa nafasi ya kushinda,” Dembele aliambia Gazeti la Le Monde.
Dembele, ambaye ni majeruhi, aliweza kuhudhuria hfla hiyo.
Kwa upande mwingine, Lamine Yamal, mwenye umri wa miaka 18 pekee, amejitokeza kama kipaji kipya cha Barcelona na alionekana kama mrithi wa Messi.
Alishinda Kopa Trophy kwa mchezaji bora mwenye umri chini ya miaka 21 kwenye gala la mwaka jana la Ballon d’Or, baada ya kuisaidia Uhispania kushinda Euro.
Yamal alifunga mabao 18 katika mechi 55 kwenye mashindano yote msimu uliopita, akisaidia Barcelona kutwaa La Liga na Copa del Rey, japokuwa walifungwa na Inter kwenye nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa.
Wachezaji tisa wa PSG waliotwaa ubingwa wa Ulaya baada ya ushindi wa kuvutia wa 5-0 dhidi ya Inter Milan waliorodheshwa kati ya wagombea 30.
Mbali na Dembele, walikuwemo pia Desire Doue, Achraf Hakimi, Khvicha Kvaratskhelia, Nuno Mendes, Joao Neves, Fabian Ruiz, Vitinha, na kipa Gianluigi Donnarumma (ambaye sasa yupo Manchester City).
Ingawa Ousmane Dembélé alikuwa hana mpinzani, tuzo ya Ballon d'Or kwa wanawake ilikuwa ya kiwango cha juu kidogo. Lakini kama ilivyokuwa miaka miwili iliyopita, kiungo wa kati wa Uhispania, Aitana Bonmati almetunukiwa tena tuzo hiyo baada ya ushindi wake wa 2023 na 2024. Mchezaji huyo wa Barcelona, ambaye alipoteza fainali zake zote mbili za Uropa (Ligi ya Mabingwa na Euro), alimshinda mtani wake, Mariona Caldeny, mshambuliaji wa Arsenal aliyeshinda Ligi ya Mabingwa dhidi ya FC Barcelona ya Bonmati.
Mshindi wa Ballon d'Or kwa wanaume: Ousmane Dembélé (Ufaransa, Paris Saint-Germain)
Mshindi wa Ballon d'Or kwa wanawake: Aitana Bonmati (Uhispania, FC Barcelona)
Kombe la Kopa (Mchezaji Bora Chipukizi): Lamine Yamal (Uhispania, FC Barcelona)
Kombe la Kopa (Mchezaji Bora Chipukizi): Vicky Lopez (Uhispania, FC Barcelona)
Tuzo ya Gerd Müller (Mfungaji Bora): Viktor Gyokeres (Sweden, Arsenal)
Tuzo ya Gerd Müller Trophy (Mfungaji Bora): Ewa Pajor (Poland, FC Barcelona)
Tuzo ya Lev Yashin (Kipa Bora): Gianluigi Donnarumma (Italia, Manchester City)
Tuzo ya Lev Yashin (Kipa Bora): Hannah Hampton (Uingereza, Chelsea)
Kocha Bora wa Wanaume: Luis Enrique (Uhispania, Paris Saint-Germain)
Kocha Bora wa Wanawake: Sarina Wiegman (Uholanzi, Uingereza)
Tuzo ya Sócrates: Xana Foundation (Hispania)
Klabu Bora ya Mwaka ya Wanawake: Arsenal (Uingereza)
Klabu Bora ya Mwaka ya Wanaume: Paris Saint-Germain (Ufaransa)