Fedha za tozo zimeingiza Sh320 bilioni katika Mfuko wa Barabara Mjini na Vijijini(Tarura).
Fedha hizo zimepatikana na hivyo zinapelekwa kwenda kumaliza migogoro na changamoto ya barabara nyingi ambazo zimekatika.
Akijibu swali la nyongeza bungeni leo Jumatatu Februari 14, 2022, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tamisemi, Innocent Bashungwa amesema fedha hizo zitafanya kazi kubwa ambayo itakuwa ni msaada kwa wananchi ambao wamekuwa na kilio cha muda mrefu.
"Kwenye tozo peke yake tumefanikiwa kukusanya zaidi ya Sh320 bilioni kwenye Tarura na bado kuna namna nyingine tunazoweza kupata fedha zaidi kwa kazi ya barabara ambayo tutaifanya vizuri," amesema Bashungwa.
Waziri amesema kwa sasa wizara hiyo imejipanga kuona Tarura inakuwa mkombozi kwa wananchi na suluhisho la matatizo kwa maeneo mengi.
Amesema kwa siku za hivi karibuni waliwaita wakandarasi wote wanaofanya kazi na Tarura pamoja na mameneja wa mikoa na wilaya ili kubainisha changamoto zilizopo.