Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Salum Nyamwese, amewataka wawekezaji wa migodi ya madini kuhakikisha wanazingatia kikamilifu kanuni na miongozo ya usalama ili kuepusha ajali zinazoweza kuzuilika.
Akizungumza wakati wa ziara ya kutembelea mgodi wa dhahabu wa GSB uliopo Kilima Mzinga, Halmashauri ya Wilaya ya Handeni, Nyamwese amesema ni jukumu la kila mwekezaji kulinda maisha ya watu pamoja na mazingira ya maeneo wanayofanyia kazi.
Amesema Wilaya ya Handeni ina hazina kubwa ya fursa za maendeleo na kwamba mshikamano wa wananchi, wawekezaji na serikali unaweza kuigeuza kuwa kitovu cha uzalishaji, ajira na ustawi wa jamii.
Katika hatua nyingine, Nyamwese amempongeza mwekezaji huyo kwa uamuzi wa kuwekeza Handeni, akibainisha kuwa hatua hiyo itafungua milango ya ajira na kuchochea maendeleo ya kiuchumi kwa wananchi.