TATIZO la utoro wa madaktari katika Kisiwa cha Pemba limepungua kwa kiwango kikubwa baada ya Serikali kuwajengea makazi ya kisasa karibu na Hospitali ya Abdalla Mzee iliyopo Mkoa wa Kusini Pemba.
Akizungumza na vyombo vya habari wakati wa ziara ya wahariri iliyoandaliwa na Kamati Maalum ya Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo ya CCM Zanzibar, Mganga Mkuu wa hospitali hiyo, Dk Hamis Suleiman Hamis, amesema uboreshaji wa mazingira ya kazi umeongeza ari na ufanisi kwa madaktari.
“Madaktari sasa wanafanya kazi kwa bidii kwa sababu hatuna haraka wala wasiwasi. Makazi yapo hapa hapa hospitalini. Tunashukuru kwa kujengewa nyumba; tunaingia na nguo tu,” alisema Dk Hamis.
Aliongeza kuwa hali ya utoaji huduma imeimarika kwa kiasi kikubwa, huku akimpongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Hussein Ali Mwinyi, kwa utekelezaji wa mradi huo wa nyumba za madaktari.
“Madaktari tunaishi maisha mazuri na hali ya afya imeimarika. Nyumba ni za kisasa, zina sehemu ya mazoezi na mazingira rafiki. Yote haya ni juhudi za Mheshimiwa Rais Mwinyi,” alisema
Kwa mujibu wa Dk Hamis, hospitali hiyo kwa sasa ina madaktari bingwa saba wa fani mbalimbali, madaktari wa kawaida 13 na wauguzi 72, ambapo kila daktari ana uwezo wa kuhudumia wastani wa wagonjwa 10 kwa siku.
Kwa upande wake, mkazi wa Uwereni, Rahima Mohammed Haji, alisema ameridhishwa na huduma bora za afya zinazotolewa kwa sasa kutokana na kuwepo kwa madaktari karibu.
“Tunashukuru Rais Mwinyi kwa kazi nzuri aliyoifanya ya kutuletea maendeleo sisi wananchi wake,” alisema Rahima