Wagombea 16 Udiwani hawana upinzani

WAGOMBEA 16 wa nafasi za udiwani kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoani Kigoma wamefanikiwa kuwa wagombea pekee baada ya vyama vingine kushindwa kusimamisha wagombea na baadhi ya wagombea wa upinzani kukosa sifa.

Katibu wa Uenezi, Siasa na Mafunzo wa CCM mkoani humo, Deogratius Nsokolo, alisema hayo jana mjini Kigoma na kubainisha kuwa hiyo ni dalili njema ya ushindi kuelekea uchaguzi wa Oktoba 29, ambapo wagombea hao wanasubiri kupigiwa kura za ndiyo au hapana.

Nsokolo alitaja kata ambazo wagombea wa CCM wamekosa wapinzani kuwa ni Wilaya ya Kasulu yenye wagombea sita, Buhigwe kata tano, Kibondo kata nne na Uvinza kata moja ya Basanza.

Kwa upande wake, Mgombea Ubunge wa Jimbo la Kasulu Mjini, Profesa Joyce Ndalichako, amesema atazindua kampeni za majukwaani Septemba 4, huku michakato mingine ya kampeni ikiendelea kabla ya mikutano ya hadhara kuanza.

Naye Mgombea ubunge wa Jimbo la Buhigwe, Profesa Pius Yanda, amesema watafanya kampeni usiku na mchana kuhakikisha ushindi wa wagombea wa chama hicho mwezi Oktoba.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii