Mgombea mwenza wa urais wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Emmanuel Nchimbi amewaeleza wananchi wa Jimbo la Itilima, Mkoa wa Simiyu kwamba maendeleo waliyopata miaka mitano iliyopita yatakuwa mara dufu mitano mingine.
Amesema ujenzi wa vituo vya afya vitatu, shule za msingi, shule za sekondari, madarasa, kuongeza upatikanaji wa majisafi ni miongoni mwa mambo wakipata ridhaa watayafanyia kazi.
Dk Nchimbi amesema hayo leo Jumanne, Septemba 2 mwaka huu katika mkutano wa kampeni za uchaguzi mkuu uliofanyika Stendi ya mabasi ya Lagangabilili, Jimbo la Itilima, Mkoa wa Simiyu.
Kampeni za uchaguzi mkuu zinaendelea kwa vyama mbalimbali kunadi ilani za vyama vyao.
Kampeni hizo zilizoanza Agosti 28 zitahitimishwa Oktoba 28 na Jumatano ya Oktoba 29 mwaka huu itakuwa ni siku ya upigaji kura kuwachagua madiwani, wabunge na Rais.