Watu saba wakiwamo askari wawili wa Jeshi la Polisi wanashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani Songwe kwa tuhuma za wizi wa mbolea yenye thamani zaidi ya Sh45 milioni iliyokuwa ikisafirishwa kutoka Dar es Salaam kwenda nchini Zambia.
Tukio la wizi huo linadaiwa kutokea Agosti 19 saa 7 hadi 8 usiku katika Kata ya Nanyala wilayani Mbozi mkoani humo, ambapo watuhumiwa hao wanadaiwa walihusika kula njama.
Akizungumza leo Septemba 2, Kamanda wa Polisi mkoani humo, Augustino Senga amesema watuhumiwa wakiwamo madereva wa treni wakishirikiana na wafanyabiashara wa mbolea kusimamisha treni hiyo 0139A mali ya Tazara.
Amesema katika tukio hilo, mifuko 534 ya mbolea hiyo aina ya Urea, yenye thamani ya zaidi ya Sh 45 mali ya kampuni ya Ocean Network ya nchini Zambia iliibwa.
“Treni hiyo ilisimamishwa eneo ambalo siyo kituo chake na kuanza kushusha mzigo, upelelezi ulianza haraka baada ya tukio hilo na kufanikiwa kuwakamata watuhumiwa saba,” amesema.
“Watuhumiwa hao wote ni wanaume, ambapo wawili ni askari wa Jeshi la Polisi (majina yamehifadhiwa kwa ajili ya upelelezi) waliokuwa wakisindikiza treni hiyo,” amesema Senga.
Kamanda huyo ameongeza kuwa baada ya doria, jeshi hilo lilifanikiwa kukamata mifuko 134 ya mbolea iliyokuwa imefichwa kijijini Iporoto kwenye nyumba ya mmoja wa watuhumiwa.