Umoja wa Afrika, umeeleza kuguswa na kuongezeka kwa fedha haramu kwenye bara hilo, fedha ambazo zimetokana na ukwepaji kodi, rushwa, utakatishaji wa fedha, utoroshaji wa mitaji na ufadhili wa ugaidi, AU ikikadiria kuwa mataifa ya Afrika hupoteza zaidi ya dola za Marekani bilioni 88 kila mwaka.
Ili kukabiliana na hili, umoja wa Afrika umechukua hatua kama vile ushirikiano baina ya Afrika na makundi ya mengine kwa lengo la kurejesha mali zilizoibwa nje ya nchi au kuchunguza sekta zilizo hatarini kama ile ya madini.
Kadhalika nchi nyingi za kiafrika zimeanzisha vitengo vya ujasusi wa kifedha na vitengo maalum vya ushuru, japokuwa ripoti hii inasema mbinu hizi hazitoshi.
Wataalam wanasema, hali hii imechangiwa na ukosefu wa ushirikiano baina ya nchi, mifumo dhaifu ya kisheria, lakini pia utegemezi wa viwango wa kigeni visivyoendana na muktadha wa bara la Afrika.