Nyambi Athuman ataja vipaumbele 13 vya maendeleo CUF

 MGOMBEA wa ubunge katika Jimbo la Morogoro Mjini kupitia Chama cha Wananchi (CUF), Nyambi Athuman amesema ilani ya chama hicho inaelekeza maeneo 13 ya vipaumbele kufanikisha Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) ifi kapo mwaka 2030.

Athuman alisema hayo wakati akizungumza kuhusu vipaumbele vya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CUF ambayo ni maalumu kwa jimbo hilo kwenye Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.

Alisema CUF katika falsafa ya Haki Sawa kwa Wote, inahakikisha kila mwananchi anapata haki zake za kiuchumi, kijamii, mazingira bora na kipato cha msingi. Athuman alisema kupitia Ilani hiyo ya uchaguzi ya mwaka huu, CUF inalenga kuongoza kwa uadilifu, ufanisi na ushirikishwaji wa wananchi katika kila hatua ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Alitaja maeneo ya vipaumbele katika ilani hiyo ni kutokomeza umasikini kwa kuwawezesha wananchi kiuchumi kupitia vikundi vya uzalishaji mali, Vyama vya Kuweka na Kukopa (SACCOS), huduma jumuishi za kifedha, kupanua ajira nadhifu kupitia programu za kilimo, biashara ndogo za kazi na viwanda vidogo na kuanzisha mpango wa ruzuku ya huduma za msingi kwa familia masikini.

Alitaja vipaumbele vingine ni kutokomeza njaa, kukuza kilimo endelevu, uboreshaji wa huduma za ugani, pembejeo za kisasa kwa wakulima, kilimo cha umwagiliaji, maeneo ya mabonde, masoko ya uhakika ya mazao kwa wakulima kupitia ushirika na mifumo ya kidijitali:

Athuman alisema ilani hiyo imeweka kipaumbele kuboresha afya njema na ustawi wa jamii, elimu bora na jumuishi, kusimamia usawa wa kijinsia na haki za kundi maalumu. Alitaja eneo lingine ni kuwezesha wananchi kupata nishati safi ya kupikia, kuongeza matumizi ya umeme wa jua kwenye shule, vituo vya afya na mitaa ya pembezoni iliyopo kwenye jimbo hilo.

Alisema pia watawezesha mazingira ya kuzalisha ajira bora na ukuaji jumuishi wa uchumi, viwanda, ubunifu na miundombinu, miji na jamii endelevu hususani kuweka mikakati ya upangaji wa miji rafiki kwa mazingira na kwa watu wa kipato cha chini.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii