“Kuanzishwa kwa Tamasha la Futopia hakumaanishi tumeliacha Sauti za Busara,” alisema Lorenzo, Mkurugenzi wa Busara Promotions, katika ufunguzi rasmi wa tamasha jipya hilo uliofanyika leo Fumba Town, Zanzibar.
Kwa miaka 22 sasa, Sauti za Busara limekuwa moja ya majukwaa makubwa na yenye mafanikio makubwa barani Afrika, likitoa fursa kwa wasanii kutoka ndani na nje ya Tanzania, pamoja na kuchangia kwa kiasi kikubwa katika kukuza uchumi kupitia utalii na burudani.
Kupitia uzoefu huo, sasa Busara Promotions wamezindua tamasha jipya lenye upekee na utofauti Futopia. Tofauti na tamasha la muziki pekee, Futopia linakuja na wigo mpana zaidi, likihusisha sanaa, tamaduni, ubunifu, na elimu ya kijamii.
“Futopia ni zaidi ya muziki pekee. Ukiwasili Fumba Town, huwezi kukosa cha kusimulia au kujifunza kuhusu tamasha hili jipya,” aliongeza Lorenzo.
Kwa mara ya kwanza, Futopia inaleta ladha mpya kwa wageni na wakazi, ikiendeleza urithi wa Sauti za Busara huku ikifungua ukurasa mpya wa ubunifu na burudani visiwani Zanzibar.