Umoja wa Vyama vya Mpira wa Miguu Ulaya (UEFA) umelainisha kanuni yake ya usajili kwa timu zinazoshiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya, uamuzi ambao unaweza kupokelewa kwa hisia chanya na klabu shiriki.
Kanuni hiyo ni ile ya kulazimisha kila timu kuwa na kikosi cha wachezaji 25 tu kutumika katika hatua ya ligi ya mashindano hayo.
Hilo limepelekea timu kuweka kando baadhi ya mastaa wao katika sajili ambazo zimewasilisha kwa UEFA na fursa pekee iliyokuwepo kwa nyota hao ni kucheza hatua ya mtoano iwapo timu hizo zitafanikiwa kuingia.
Lakini hata hivyo UEFA imelegeza kwa kuongeza kipengele cha kuruhusu klabu kuingiza jina la mchezaji wakati hatua ya ligi ikichezwa iwapo kutakuwa na mchezaji katika kikosi cha watu 25 kilichosajiliwa, atapata majeraha au ugonjwa utakaomfanya akae nje ya uwanja kwa muda mrefu.
Kanuni hiyo itatumika hadi katika mechi ya sita ya hatua ya ligi ya mashindano hayo katika muda ambao hatua ya makundi ya mashindano ya Conference League itakuwa inafikia tamati.
Taarifa iliyotolewa na UEFA imeleeza kwamba uamuzi huo unalenga kulinda wachezaji.