Bandari ya Mtwara yazidi kung’ara kimataifa

 SERIKALI ya Urusi imeonyesha nia ya kutumia Bandari ya Mtwara kusafirisha bidhaa zake na kuzisambaza katika nchi jirani na Tanzania, ikiwemo kusafirisha korosho kwenda soko la Urusi.

Balozi wa Urusi nchini Tanzania, Andrey Avetisyan, amesema hayo wakati alipotembelea Bandari ya Mtwara kuangalia fursa za biashara na uwekezaji mkoani humo akiwa ameambatana na ujumbe kutoka ubalozi huo, Amesema Urusi ina bidhaa nyingi zinazoweza kusafirishwa kupitia bandari hiyo kwenda nchi za Afrika Mashariki na Kusini, ikiwemo mbolea na bidhaa za nishati.

Kwa mujibu wa Avetisyan, Bandari ya Mtwara imeboreshwa na ina nafasi kubwa kutokana na eneo lake la kijiografia, kwani inapakana na nchi ambazo hazina bahari, hivyo ni rahisi kuhudumia shehena kutoka Urusi. Kwa upande wake,Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Patrick Sawala, amepongeza hatua hiyo akisema itasaidia kutangaza bandari kimataifa na kuinua uchumi wa mkoa.

Balozi Avetisyan pia alitembelea Kongani la Viwanda la Mranje na kufanya mazungumzo na viongozi wa mkoa pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Korosho Tanzania (CBT), Alfred Francis. 

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii