Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya DCEA imekamata kemikali hatarishi kwenye bangi aina ya THC, ambapo zikichanganywa na bangi na kuvutwa na mwanamke mjamzito mimba hutoka ama kuharibika.
Kamishina Jenerali wa DCEA, ARETAS LYIMO amesema kemikali ambazo zina madhara kiafya ikiwemo kwa mama wajawazito ni Benzene na Madini ya cadmium, Lead na Mekyuri ambazo zikitumika pia husababisha magonjwa ya akili, saratani, kusababisha udumavu wa akili baada ya mtoto kuzaliwa na hivyo kuathiri uwezo wa kujifunza pamoja na uraibu.
Kamishina LYIMO amesema hayo wakati akitoa taarifa ya operesheni ambayo mamlaka yake imefanya mwezi Julai na Septemba Saba mwaka huu, ambapo huko Jijini Dar es Salaam
kwenye klabu ya “Bad London” na klabu ya “Sanaa” Masaki, sigara za kielektroniki (e sigaret) pisi 50 zilizotengenezwa kwa kutumia kemikali ya THC pamoja na skanka ziliingizwa nchini kutokea Uingereza.
Katika tukio lingine mkoani humo, Simoni Gervas Mkonda (51) amekamatwa akiwa na kilogramu 193 za bangi pamoja na silaha aina ya bastola ikiwa na risasi 11 ambayo amekuwa akiimiliki kinyume cha sheria akiitumia kulinda biashara zake haramu.