Mawakili wa Chama cha ACT -Wazalendo na wale wa Serikali wameshaingia na kuketi kwenye viti vyao mahakamani tayari kwa ajili ya kesi ya Luhaga Mpina aliyeenguliwa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kuwania kiti cha urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
Leo Jumatatu Septemba 8 mwaka huu katika Mahakama Kuu Masijala Kuu- Dodoma, majaji wanatarajiwa kutoa hukumu ya kesi hiyo ambayo imebeba hatima ya ACT -Wazalendo kama watakuwa na mgombea urais au watakosa.
Shauri hilo linalosikilizwa na jopo la majaji watatu, Abdi Kagomba (kiongozi wa jopo), Evaristo Longopa na John Kahyoza lilipangwa leo kwa ajili ya uamuzi.
Mpina aliyepitishwa na ACT – Wazalendo kugombea urais amefungua shauri kupinga kuenguliwa na INEC katika orodha ya walioomba kuteuliwa kuwania nafasi hiyo.
Kabla ya mawakili wa ACT - Wazalendo kuingia mahakamani hapo, walitanguliwa na mawakili wa Serikali walioingia mapema na kuanza kupekua makabrasha, dalili za kuwa wanapitia vifungu vya sheria.