ACT yazindua kampeni kwa kishindo mkoani Kigoma

MGOMBEA ubunge wa Jimbo la Kigoma Kaskazini kupitia Chama cha ACT-Wazalendo, Kiza Mayeye amezindua rasmi kampeni zake akiahidi kusimamia vipaumbele vitano vya maendeleo kwa wananchi wa jimbo hilo.

Akizungumza katika viwanja vya soko la Mwandiga, Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma, Mayeye alisema atajikita katika kuboresha huduma za afya, kuhakikisha upatikanaji wa elimu bora na nafuu, sambamba na kuimarisha huduma za maji safi na salama karibu na makazi ya wananchi.

Alivitaja vipaumbele vingine kuwa ni uboreshaji wa miundombinu ya barabara zinazofungua fursa za uchumi na kilimo pamoja na kuwezesha vijana na wanawake kupitia mazingira bora ya kiuchumi na kijamii. 

Akihitimisha mkutano huo, Mayeye alikumbusha kuwa mwaka 2020 alipata kura nyingi lakini hakutangazwa mshindi, akitoa wito kwa wasimamizi wa uchaguzi kuhakikisha uchaguzi wa mwaka huu unakuwa huru na haki.

Kwa upande wake, Kiongozi Mstaafu wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe alisema chama kimeamua kumsimamisha Mayeye kutokana na sifa, uthubutu na uwezo wake wa kuwatumikia wananchi.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii