Askari wanne mbaroni kwa kuua raia

Jeshi la Polisi Mkoa wa Geita linawashikilia askari wanne wa Hifadhi ya Kigosi iliyoko Wilaya ya Bukombe kwa tuhuma za mauaji ya kijana Hezron Fikiri (20), mkazi wa Kijiji cha Msonga.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Adam Maro, alisema tukio hilo lilitokea Agosti 13, mwaka huu majira ya asubuhi, baada ya sintofahamu iliyozuka baina ya askari hao na baadhi ya wananchi waliodaiwa kuingia hifadhini bila vibali halali.

Baada ya watu hao kuingia kwenye hifadhi hiyo bila kufuata taratibu, mmoja wa askari alifyatua risasi na kumpata kijana huyo, hali iliyosababisha kifo chake,” alisema Kamanda Maro na kuongeza kuwa uchunguzi wa kina unaendelea kabla ya hatua zaidi za kisheria kuchukuliwa.
Tukio la Pili: Wananchi 50 Wakamatwa.

Katika tukio jingine, Jeshi la Polisi linawashikilia watu 50 kwa tuhuma za kujichukulia sheria mkononi baada ya kuchoma shamba la miti na majengo ya Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) yaliyoko Kitongoji cha Rwamgasa, Wilaya ya Geita, pamoja na kuwashambulia kwa kipigo baadhi ya askari.
Kamanda Maro alisema tukio hilo lilitokea Agosti 13, mwaka huu majira ya mchana na kwamba watuhumiwa wanaendelea kuhojiwa huku uchunguzi ukiendelea ili kubaini chanzo na wahusika zaidi.
Malalamiko ya Wananchi.

Baadhi ya wakazi wa kitongoji hicho walidai kuwa chanzo cha vurugu hizo ni kitendo cha askari wa TFS kuwakamata watoto wawili waliokuwa wameingia hifadhini kukusanya kuni na kuwaadhibu. Aidha, walidai askari hao wamekuwa wakijihusisha na vitendo vya unyanyasaji ikiwemo ubakaji dhidi ya wanawake na watoto wanaopita katika eneo hilo.

Wakazi hao waliiomba serikali kuwapangia maeneo maalumu kwa ajili ya shughuli za kilimo na ufugaji ili kuepusha migongano ya mara kwa mara na askari wa hifadhi.

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kitongoji cha Rwamgasa, Bahati Charles, alithibitisha kupokea malalamiko ya mara kwa mara kutoka kwa wananchi kuhusu ukatili wanaodai kufanyiwa na askari wa TFS.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii