Idara ya huduma za uokoaji zinajaribu kutafuta zaidi ya watu 40 ambao hawajulikani waliko baada ya ajali ya boti kaskazini magharibi mwa Nigeria siku ya Jumapili jioni, Agosti 17, Mamlaka ya kitaifa ya masuala ya dharura nchini Nigeria, NEMA limetangaza.
Zaidi ya watu 40 hawajulikani walipo baada ya ajali ya boti nchini Nigeria. Boti hiyo, iliyokuwa na watu 50 kuelekea soko maarufu katika Jimbo la Sokoto, kaskazini-magharibi mwa nchi, ilipinduka siku ya Jumapili, Mamlaka ya kitaifa ya masuala ya dharura nchini Nigeria, NEMA, imesema.
"Takriban watu kumi wameokolewa, huku zaidi ya abiria 40 wakiwa hawajulikani walipo," NEMA imesema katika taarifa, ikibainisha kuwa ajali hiyo imetokea katika Jimbo la Sokoto.
Abiria walikuwa wakielekea Soko la Goronyo, soko kubwa la vyakula katika jimbo hilo, wakati boti hiyo ilipopinduka. Watu kumi waliokolewa, amesema Zubaidar Umar, mkurugenzi wa Mamlaka ya kitaifa ya masuala ya dharura nchini Nigeria, NEMA, katika taarifa iliyochapishwa kwenye mtandao wa kijamii wa X.
Shirika hilo liliongeza kuwa linashirikiana na mamlaka za eneo hilo na idara ya huduma za dharura katika operesheni ya kuwatafuta na kuwaokoa watu waliotoweka.
Wiki tatu zilizopita, takriban watu 13 walifariki na makumi ya wengine hawajulikani walipo baada ya boti iliyokuwa imebeba takriban abiria 100 kupinduka katika Jimbo la Niger, kaskazini-kati mwa Nigeria.