Mtunzi na mwimbaji wa nyimbo za mbalimbali za hamasa za Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), ikiwemo ya ‘Tundu Lissu wapeleke mchakamchaka’, George Mwingira amefariki dunia baada ya kupata ajali ya gari.
Kwa mujibu wa Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Kanda ya Kusini, Belle Ponera, Mwingira amefariki dunia Jumapili Agosti 10, 2025 maeneo ya Mikumi mkoani Morogoro baada ya basi alilokuwa amepanda kutoka Songea, Mkoa wa Ruvuma kwenda Dar es Salaam kupata ajali.
Nyimbo nyingine ambayo Mwingira, maarufu ‘MC Mwingira’ amewahi kutamba nayo ni pamoja na ‘No reforms no election’ ambayo ndio ilikuwa kibao chake cha mwisho kukitoa kabla ya kufariki dunia.
Kufutia kifo hicho Chadema kinaendelea kupata pigo kwa wasanii wake kufariki dunia, ambapo kabla ya Mwingira, Fulgence Mapunda ‘Mwanacotide’ alifariki dunia mwaka 2019 aliyewahi kutamba na nyimbo za ‘Chadema People’s Power’ na ‘Polisi msitupige mabomu Chadema’, akafuata Sara Alex aliyetamba na wimbo ‘Mwamba tuvushe’ aliyefariki dunia mwaka 2022.
Akizungumza na Mwananchi leo Alhamisi Agosti 14 mwaka huu onera amesema; ”Mwingira alikuwa anasafiri kwenda Dar es Salaam, kuhudhuria kesi ya Tundu Lissu (mwenyekiti wa Chadema), tulikuwa tuna mawasiliano naye mazuri lakini ghafla yalikata.”