Bandari Kavu ya Kwala yazinduliwa rasmi leo

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan leo Alhamisi Julai 31, 2025 amekagua na kuzindua rasmi Bandari Kavu ya Kwala mkoani Pwani pamoja na kupokea mabehewa mapya na yaliyokarabatiwa ya reli ya kati Meter-Gauge Railway (MGR).

Miradi yote hiyo ni kielelezo na uthibitisho wa dhahiri wa maono ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha Tanzania inapiga hatua kubwa za kimaendeleo kwa kutumia fursa zilizopo, ikiwemo kuzungukwa na nchi jirani ambazo zinategemea Bandari za Tanzania kama lango lao kuu la biashara ikiwemo Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ambazo zimetengewa maeneo maalum ya kuhifadhi mizigo katika bandari hiyo.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) Bw. Plasduce Mbossa amemueleza Rais Samia kuwa Bandari hiyo Kavu ya Kwala inatarajiwa kupunguza muda na gharama za usafirishaji wa mizigo pamoja na kupunguza msongamano wa magari kwenye Jiji la Dar Es Salaam.

Mbossa pia ameeleza manufaa mengine kuwa ni pamoja na kuchochea uwekezaji na uanzishaji wa viwanda katika Ukanda wa Kwala pamoja na kuongeza mapato ya serikali kupitia huduma ya bandari, akisema eneo zima la bandari hiyo linafikia hekta 502, mara tano zaidi ya bandari ya Dar Es Salaam huku pia bandari hiyo ikiunganishwa na Reli ya Kisasa ya SGR, bandari ya Bagamoyo, Reli ya Kati na Reli ya TAZARA.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii