Kenya yapiga marufuku unywaji wa pombe chini ya miaka 21

Serikali ya Kenya imetangaza kupiga marufuku uuzwaji wa pombe katika maeneo mbalimbali ya wazi nchini humo kama kwenye fukwe, bustani za kupumzika, vituo vya huduma za afya, vituo vya mabasi, vituo vya mafuta, vituo vya reli na kwenye usafiri wa umma kama treni, feri na kwenye barabara kuu. Supermarket, migahawa na huduma za kuuza bidhaa mitandaoni pia imepigwa marufuku kuuza pombe.

Sambamba na hilo, umri wa kunywa pombe umepandishwa kuwa miaka 21 tofauti na 18 hapo awali, ambapo mtu yeyote mwenye umri wa miaka chini ya 21 hataruhusiwa kuingia duka au eneo linalouza vilevi akiwa peke yake au akiwa amesindikwa na mtu mzima.

Katika hatua nyingine marufuku hiyo imewagusa watu maarufu ikiwemo wanamichezo ambao wamepigwa marufuku kuwa mabalozi au kutangaza bidhaa za vilevi na madawa ya kulevya. 

Taarifa iliyotolewa na Mamlaka ya Kampeni Dhidi ya Pombe na Matumizi ya Dawa (NACADA) imesema hatua hiyo ni kukabiliana na athari za unywaji pombe holela miongoni mwa vijana unaopelekea athari kubwa.

“Sera hii imeshirikisha wadau mbalimbali nchini, kama mamlaka za majimbo, asasi za kiraia, makundi ya kidini, sekta binafsi na jamii kwa ujumla. Kwa pamoja tumetengeneza mkakati wa kudhibiti na kuzuia madhara makubwa ya matumizi ya hovyo ya vilevi na dawa kwenye taifa letu”, amesema Onesimus Kipchumba Murkomen, Katibu wa Wizara Mambo ya Ndani na Utawala.


Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii