Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, leo Alhamisi ameweka jiwe la msingi katika Kongani ya Viwanda ya Kwala, iliyopo mkoani Pwani, ikiwa ni sehemu ya juhudi za serikali kukuza uchumi wa viwanda nchini.
Katika tukio hilo la kihistoria, Rais Samia pia amezindua rasmi usafirishaji wa mizigo kupitia reli ya kisasa ya Standard Gauge Railway (SGR) katika Bandari Kavu ya Kwala, hatua inayolenga kuongeza ufanisi wa usafirishaji wa mizigo kutoka bandari ya Dar es Salaam kwenda maeneo mbalimbali ya nchi na ukanda wa Afrika Mashariki.
Kongani ya Viwanda ya Kwala inatarajiwa kuwa kitovu kikubwa cha viwanda vya kuchakata bidhaa mbalimbali na imeunganishwa moja kwa moja na reli ya SGR, hivyo kurahisisha usafirishaji wa malighafi na bidhaa za viwandani kwa haraka na kwa gharama nafuu.
Ujenzi wa bandari kavu ya Kwala na reli ya SGR ni sehemu ya ajenda ya Tanzania ya kukuza uchumi kupitia uwekezaji mkubwa kwenye miundombinu ya kisasa, ikiwemo reli, barabara, bandari na maeneo ya viwanda.