WAZIRI Mkuu wa Canada, Mark Carney, ametangaza kuwa nchi yake inapanga kulitambua rasmi Taifa la Palestina katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwezi Septemba mwaka huu.
Tangazo hilo linakuja siku chache baada ya mataifa ya Ufaransa na Uingereza pia kueleza nia yao ya kulitambua taifa hilo, jambo ambalo linaongeza shinikizo kwa Israel kuafiki suluhisho la mataifa mawili.
Carney amesema Canada imefikia hatua hiyo kufuatia hakikisho lililotolewa na Mamlaka ya Palestina kuwa iko tayari kufanya uchaguzi mwaka 2026, ambao hautahusisha kundi la Hamas.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Israel imekosoa vikali uamuzi huo wa Canada, huku Rais wa Mamlaka ya Palestina, Mahmoud Abbas, akieleza kuwa ni hatua ya kihistoria kwa harakati za Wapalestina kupata taifa huru.