Mzee wetu Hemed Morocco na benchi lake la ufundi wanastahili pongezi nyingi sana kwa ambacho wanakifanya kwenye fainali za CHAN 2024! Tusisubiri mambo yaende ndivyo sivyo ili tutoe maneno makali kwao na kuwachambua wao.
Kwa mara ya kwanza Tanzania imefuzu hatua ya mtoano [robo fainali] kwenye fainali za CHAN baada ya kuvuna alama tisa [9] kwenye michezo mitatu ya Kundi B tena ikiwa na mchezo mmoja umesalia kwenye hatua ya makundi.
Sikumbuki ni lini Taifa Stars imeshinda michezo mitatu mfululizo kwa siku za hivi karibuni! Chini ya Morocco hilo limewezekana na sasa robo fainali ya CHAN 2024 ipo mbele yake kuikabili.
Tuwasifie vijana wetu kwa maana ya wachezaji kwa namna wanavyojitoa uwanjani kupigania ushindi lakini kamwe tusisahau kuwapa heshima yao watu wa benchi la ufundi wakiongozwa na Hemed Morocco kwenye kile kizuri ambacho wanakifanya kupitia CHAN 2024.