Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Mamlaka ya kusimamia Uvuvi wa Bahari Kuu (DFSA) imefanikiwa kudhibiti vitendo vya Uvuvi haramu kwenye ukanda wa Bahari Kuu wenye kilomita za mraba 223,000 kwa kutumia vifaa vilivyounganishwa kupitia teknolojia ya kisasa.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo Dkt. Emmanuel Sweke alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma.
“Tuna mfumo wa kutambua meli zote kwa haraka ambao unatuwezesha kufahamu Meli ambazo hatuzitambui, hazijakata leseni au hazina vibali na kwa utaratibu meli yoyote ile iliyosajiliwa inapaswa kutoa taarifa saa 24 kabla ya kuingia baharini” Amesema Dkt. Sweke.
Aidha Dkt. Sweke amebainisha kuwa mamlaka yake imekuwa ikifanikisha jukumu hilo la ulinzi wa rasilimali za Uvuvi wa bahari kuu kwa kushirikiana na kamisheni ya Jodari ya Bahari ya Hindi na kamisheni ya bahari ya Hindi iliyopo nchini Mauritania ambayo hushirikiana nayo kufanya doria ya pamoja kwenye ukanda huo.