Tanzania na Canada zimekubaliana kuendelea kushirikiana katika kuimarisha sekta ya elimu ya ualimu, ufundi na mafunzo ya ufundi stadi, kupitia miradi mbalimbali inayolenga kutoa ujuzi na kuongeza ubora wa elimu nchini.
Makubaliano hayo yamefikiwa jijini Dodoma katika kikao baina ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia wa Tanzania, Prof. Adolf Mkenda na Waziri wa Maendeleo ya Kimataifa wa Canada, Mhe. Randeep Sarai.
Prof. Mkenda amesema kuwa katika kikao hicho, wamejadili kwa kina kuhusu miradi ya pamoja iliyopo, changamoto zake, na namna ya kuimarisha ushirikiano hasa katika kutoa fursa za mafunzo ya ufundi na ualimu kwa Watanzania ndani na nje ya nchi, hususan nchini Canada.
“Canada imekuwa mshirika wa karibu katika maendeleo ya elimu nchini, ambapo miradi mbalimbali ya kuboresha elimu ya ualimu na mafunzo ya ufundi imekuwa ikiungwa mkono kwa ufadhili wa fedha na kiufundi,” amesema Prof. Mkenda.
Miongoni mwa miradi inayotekelezwa kwa ufadhili wa Serikali ya Canada ni pamoja na Mradi wa Kuendelea Elimu ya Ualimu (TESP) wenye thamani ya Shilingi Bilioni 92, Mradi wa Uwezeshaji kupitia Ujuzi (ESP) wenye thamani ya Shilingi Bilioni 47 na Mradi mpya wa Maendeleo Endelevu katika Elimu ya Ualimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (TESDP) utakaogharimu takriban Shilingi Bilioni 37.
Kwa upande wake, Mhe. Sarai amesema Canada itaendelea kuwekeza katika maeneo muhimu ya kijamii kupitia sekta ya elimu, ikiwemo mpango wa Lishe Shuleni utakaogharimu Dola za Kimarekani Milioni 12, ili kuongeza uandikishaji na ufaulu wa wanafunzi, sambamba na mradi wa BLOOM wenye lengo la kuwawezesha wanawake na wasichana kupitia VETA kwa gharama ya Dola za Kimarekani Milioni 20.