Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam SACP Jumanne Muliro amesema hakuna msingi wa kisheria wa kuzuia uchaguzi kwa kutumia kauli ya “No Reform No Election”, akisisitiza kuwa Jeshi la Polisi linasimamia sheria, siyo kauli za kisiasa.
Akizungumza vyombo vya habari siku ya leo julai 22 Kamanda Muliro amesema kuwa Kwenye sheria hakuna sehemu ambapo pameandikwa kwamba uchaguzi utazuiwa labda kwa kitu kinaitwa au sheria inaitwa No Reform No Election. Sisi ni wasimamizi wa sheria. Ukisema utazuia uchaguzi kwa sheria ipi? Kwa slogan hiyo? Mimi ni msimamizi wa sheria, wewe unasema No Reform No Election, ninakushangaa!
Kauli hiyo imekuja wakati ambapo mijadala ya kisiasa imepamba moto kuhusu uhitaji wa marekebisho ya mfumo wa uchaguzi kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025. Hata hivyo, Kamanda Muliro ameeleza kuwa hoja hizo hazipaswi kutumiwa kama msingi wa kuvuruga mchakato wa kidemokrasia ambao unaongozwa na Katiba na sheria za nchi.
Aidha Kamanda Muliro amegusia mjadala unaoibuka mara kwa mara kuhusu askari polisi kujitambulisha au kutaja kosa la mtuhumiwa wakati wa kumkamata. Amesema utekelezaji wa sheria unategemea mazingira ya tukio husika.
“Unasema askari hajajitambulisha. Lakini mazingira yanasemaje? Kama mhalifu ana panga au silaha na anaanza kukimbia, askari atajitambulisha vipi? Au unataka amweleze kosa lake wakati yuko tayari kumshambulia? Anaweza kuwa tayari ameshakata mkono kabla hata ya kusikia kosa lake.”
Ameeleza kuwa, kwa kawaida, sheria inataka askari ajitambulishe, amtaje mtuhumiwa kosa lake na kumpeleka kituoni, lakini katika mazingira hatarishi, askari hulazimika kutumia mbinu za haraka ili kujilinda na kuhakikisha usalama.
Kamanda Muliro ametoa wito kwa wananchi wa Dar es Salaam kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi na wadau wengine wa usalama. Amesema Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP) Camillus Wambura ameweka msisitizo mkubwa juu ya nidhamu, haki za binadamu, na uadilifu kwa askari wote.
"Wananchi wawe na imani na jeshi lao, na Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP Camilius Wambura anafuatilia sana suala la nidhamu, uweledi, uadilifu na haki za wananchi kuliko watu wanavyofuatilia".