TANZANIA imeahidi kuunga mkono
utekelezaji wa Awamu ya Pili ya Programu ya Kikanda ya Hifadhi ya
Mazingiraya Bonde la Ziwa Tanganyika kutokana na umuhimu wa program hiyo
kwa wananchi wa nchi nne zinazonufaika na program hiyo ikiwemo
Tanzania, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia Congo, Rwanda na Zambia.
Ahadi
hiyo imetolewa Jijini Dodoma na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na
Mipango, Bw. Emmanuel Tutuba, alipokutana na kufanya mazungumzo na
Ujumbe wa Sekretarieti ya Mamlaka ya Ziwa Tanganyika (LTA) uliofika
ofisini kwake kuomba idhini ya Serikali ya kuanza kutafuta fedha kwa
ajili ya utekelezaji wa mradi huo.
Alisema kuwa Serikali inaunga
mkono kuanza kwa Awamu ya Pili ya Programu ya Kikanda ya Hifadhi ya
Mazingira ya Bonde la Ziwa Tanganyika (PRODAP II) baada ya Awamu ya
kwanza ya program hiyo iliyokamilika mwaka 2014 kuwa na manufaa makubwa
kwa wananchi wanaozunguka Bonde la Ziwa Tanganyika katika nchi hizo nne
za Kikanda.
“Katika kuandaa mradi wa awamu ya pili tumekubaliana
kuwa sisi kama Wizara ya Fedha na Mipango tutaratibu Wizara nyingine ili
tupate vipaumbele ambavyo tutaviwasilisha katika Taasisi yake ili iweze
kuviunganisha na vile vya nchi wanachama kisha kuiwasilisha katika
Benki ya Maendeleo ya Afrika ili waweze kufanya upembuzi yakinifu ili
miradi hiyo ikitekelezwa iweze kuwiana na malengo ya kupunguza umasikini
kwenye jamii inayozunguka eneo hilo” alisema Bw. Tutuba.
Alisema
kuwa katika Awamu ya kwanza, Mamlaka ya Hifadhi ya Ziwa Tanganyika
ilitekeleza mradi wa ujenzi wa masoko eneo la Kibirizi Mkoani Kigoma
ambapo wameweka vifaa mbalimbali vya uhifadhi wa Samaki na Dagaa, maeneo
ya kukaushia Samaki na maghala ya kuhifadhia samaki.
Bw. Tutuba
alisemakuwa miradi mingine iliyotekelezwa ni ujenzi wa vyumba vya
madarasa katika shule 22, Vyoo kwenye shule 18, miradi mitano ya vituo
vya afya, nyumba za watumishi kwenye vijiji viwili na Zahanati moja na
miradi 10 ya maji katika vijiji vinavyozunguka Ziwa Tanganyika.
Miradi
mingine ni ujenzi wa kilomita 65.6 za barabara, madaraja mawili na
kufanya kampeni 180 za kujikinga na magonjwa ya kuambukiza ukiwemo
Ukimwi.
Aidha, Bw. Tutuba alisema kuwa katika awamu ya kwanza ya
utekelezaji wa programu hiyo, Tanzania imekuwa ikichangia kila mwaka
dola 303,900 ambapo kiwango hicho kinachangiwa na kila nchi mwanachama
na kwamba miradi hiyo imechangia kwa kiasi kikubwa kuchochea ukuaji wa
uchumi wa nchi na kupunguza umasikini kwa wananchi.
Bw. Tutuba
alisema kuwa Tanzania iko tayari kuendelea na utekelezaji wa Awamu ya
Pili ya Programu hiyo kutokana na fedha zitakazopatikana kwa njia ya
mkopo nafuu kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) kwa kuwa miradi
iliyotekelezwa kupitia ushirikiano huo imeleta maendeleo uendelevu ya
Mazingira katika Ziwa Tanganyika na inagusa sekta mbalimbali za kuondoa
umasikini kwa wananchi.
Naye Balozi wa Tanzania nchini Burundi,
ambaye anasimamia maslahi ya Tanzania katika Sekretarieti ya Mamlaka ya
Ziwa Tanganyika yenye Makao yake Makuu nchini Burundi, Mhe. Dkt. Jilly
Maleko, alisema kuwa Lengo la ziara ya Sekretarieti hiyo nchini ni
kufanya mazungumzo kuhusu uwezekano wa kupata mkopo kutoka Benki ya
Maendeleo ya Afrika (AfDB) kwa ajili ya kutekeleza awamu ya pili ya
Programu ya Kikanda ya Uhifadhi wa Mazingira ya Bonde la Ziwa Tanganyika
(PRODAP II).
Alisema kuwa awamu ya kwanza ya mradi huo ambayo
ilimalizika mwaka 2014, kwa upande wa Tanzania ulitekelezwa chini ya
uratibu wa Ofisi ya Makamu wa Rais kwa gharama za dola za Marekani
milioni 7.2 kupitia ufadhili wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB).
Alisema
kuwa Mamlaka ya LTA imefanya mazungumzo na AfDB kuhusu uwezekano wa
kutekelezwa kwa PRODAP II kwa msaada au Mkopo wa masharti nafuu na
tayari Sekretarieti hiyo imefanya mazungumzo na Jamhuri ya Kidemokrasia
ya Kongo, Burundi na Zambia ambazo zimeonesha nia ya kuendelea na
utekelezaji wa programu hiyo kwa awamu ya pili.
Kwa upande wake
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Ziwa Tanganyika, Bw. Tusang Sylvain
Tusanga, alizishukuru nchi wanachama hususani Tanzania kwa kuonesha nia
thabiti ya utekelezaji wa miradi hiyo na kutoa michango yake ya kila
mwaka kikamilifu tangu mwaka 2000.
Alisema ushirikiano huo
umeleta tija katika Bonde la Ziwa Tanganyika na kufanikisha utekelezaji
wa miradi mbalimbali ikiwemo ya ujenzi miundombinu ya barabara, afya,
elimu, uvuvi na hifadhi ya mazingira