Marcus Rashford rasmi ni mchezaji wa Barcelona, na tayari amekabidhiwa jezi namba 14 namba yenye historia kubwa katika klabu hiyo, ikiwa ni kumbukumbu ya gwiji wa soka, Thierry Henry.
Akizungumza baada ya kukabidhiwa jezi hiyo, Rashford amesema:"Namba hii ina uzito mkubwa hapa. Ni heshima kubwa sana kupewa nafasi ya kuvaa namba aliyowahi kuvaa Thierry Henry. Najua majukumu yake na nitajitahidi kulinda heshima yake."
Katika mkutano wake wa kwanza na waandishi wa habari wa Hispania, Rashford aliulizwa maswali kadhaa kuhusu maisha yake mapya, uamuzi wa kujiunga na Barcelona, na kuondoka kwake Old Trafford.
“Sitaki kusema vibaya kuhusu Manchester United. Ni klabu iliyonilea, imenipa jukwaa la kuonyesha uwezo wangu na itanibaki kuwa sehemu muhimu ya maisha yangu. Lakini maisha huenda kwa hatua na huu ni mwanzo mpya.”
Alipoulizwa kuhusu sakata la kuachwa nje ya kikosi cha kwanza chini ya kocha Ruben Amorim kabla ya kuondoka United, Rashford hakutaka kulizungumzia kwa kina.
Kwa sasa, macho yote yako kwa Rashford si tu kwa uwezo wake wa kufunga na kusaidia, bali pia kwa jinsi atakavyobeba jukumu la kuvaa jezi namba 14 yenye uzito.