Vijana kupatiwa mafunzo ya Ujasiriamali na ajira

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Adolf Mkenda amezindua rasmi Programu ya Mafunzo ya Ujasiriamali na Ajira, inayolenga kuwasaidia vijana kutoka vyuo viwili vya VETA na chuo kimoja cha Maendeleo ya Wananchi (FDC). 

Akizungumza katika uzinduzi huo uliofanyika mkoani Dar es Salaam, Profesa Mkenda amebainisha kuwa programu hiyo kwa awamu ya kwanza itajumuisha vijana 200, na inalenga kupunguza tatizo la ajira kwa vijana ambao licha ya kuwa na maarifa ya kitaaluma, hukosa ujuzi wa vitendo unaohitajika kwenye soko la ajira pamoja na mitaji ya kuanzisha biashara.

Amesisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano kati ya taasisi za elimu na viwanda ili kuwezesha vijana kupata ujuzi wa vitendo.

Ameongeza kuwa ni muhimu kuendeleza urasimishaji wa maarifa waliyonayo wafanyabiashara katika maeneo mbalimbali na kushirikiana nao katika kufundisha vijana ili kuwapa maarifa na ujuzi utakaowawezesha kushiriki katika ajira au kujiajiri.

Programu hiyo ya Mafunzo ya Ujasiriamali na Ajira, ni sehemu ya juhudi za Serikali kushirikiana na wadau wa elimu na maendeleo katika kuhakikisha vijana wanapata fursa za kujifunza, kubuni, na kuchangia kikamilifu katika uchumi wa Taifa.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii