Kesi ya mgawanyo wa rasilimali za Chama cha Demokrasia na Maendeleo inatarajiwa kuendelea leo Julai 10, 2025 katika Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Dar Es Salaam ambapo leo itasikilkzwa kesi ya msingi.
Wadai katika kesi hiyo iliyo mbele ya jaji Hamidu Mwanga imefunguliwa na Said Issa Mohamed, Makamu Mwenyekiti mstaafu wa chama hicho Taifa, Zanzibar, Ahmed Rashid Khamis na Maulida Anna Komu, ambao ni wajumbe wa Bodi ya Wadhamini wa chama hicho kutoka Zanzibar.
Huku Wadaiwa wakiwa ni Bodi ya Wadhamini wa CHADEMA na Katibu Mkuu wa chama hicho ambao sio wanadaiwa kutozitumia rasilimali za chama kwa usawa huku upande wa bara ukipendelewa zaidi.
Ikumbukwe kesi hii ilipangwa kuanza kusikilizwa juni 24, 2025 lakini iliahirishwa kutokana na jaji(Mwanga) kutokuweza kufika mahakamani.
Hata hivyo viongozi wa chama hicho akiwemo Kaimu Katibu Mkuu John Mnyika walimuomba Jaji Hamidu Mwanga kujitoa katika kusikiliza kesi yao kwa kile walichodai kuwa wanadhani hatowatendea haki.
Mara ya mwisho shauri hili kusikilizwa mbele ya Jaji Mwanga ilikuwa Juni 10, ambapo yalikuwa yanasikilizwa mapingamizi ya upande wa wajibu maombi (walalamikiwa) waliowakilishwa na Wakili Jebra Kambole ambapo mahakama ilitupilia mbali mapingamizi yote tisa ya CHADEMA.
Siku hii iliacha kumbukumbu chungu kwa CHADEMA kwani Wakili Jebra alijiondoa kwenye kesi na kesi iliendelea kusikilizwa kwa upande mmoja ambapo mahakama ilitoa uamuzi wa shauri dogo lililofunguliwa na walalamikaji juu ya kutaka CHADEMA kusimama shughuli zake. Ambapo chama hicho kilizuiliwa kuendelea na shughuli zake kwa kutumia rasilimali za chama mpaka pale kesi ya msingi itakapotolewa uamuzi.