Aliyekuwa kipa wa Simba SC na timu ya taifa, Taifa Stars, Aishi Salum Manula, amerejea rasmi katika klabu yake ya zamani ya Azam FC baada ya kusaini mkataba wa miaka minne utakaomuweka kambini hadi mwaka 2028.
Manula, ambaye alianza safari yake ya soka la kulipwa kupitia Azam FC kabla ya kutimkia Simba SC , ameamua kurudi nyumbani kuendelea na safari yake ya soka.
Kupitia katika klabu ya Simba Manula aliweka historia ya kutwaa mataji mbalimbali ya Ligi Kuu Tanzania Bara, FA Cup na kufika hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, akijizolea heshima kama mmoja wa makipa bora zaidi kuwahi kutokea Tanzania.
Katika taarifa yao, Azam FC wamesema wamemrudisha Manula kwa lengo la kuimarisha safu yao ya ulinzi kuelekea msimu mpya wa mashindano ya ndani na kimataifa.
Manula anatarajiwa kuungana na kikosi cha Azam FC mara moja kuanza maandalizi ya msimu mpya wa 2025/2026.