Klabu ya Liverpool ya England inaendelea kuweka juhudi zake za kumtia mikononi mshambuliaji chipukizi Hugo Ekitike kutoka Eintracht Frankfurt ya Ujerumani, katika dirisha hili la usajili la majira ya kiangazi.
Kwa mujibu wa taarifa za karibu na mazungumzo hayo, Liverpool imeingia katika hatua za mbele za mazungumzo ya moja kwa moja kati ya klabu na klabu (club-to-club talks) na Frankfurt, wakilenga kufikia makubaliano rasmi juu ya dau la uhamisho wa mchezaji huyo mwenye miaka 22.
Huku kukiwa na hali ya sintofahamu kuhusu uwezekano wa kumsajili Alexander Isak kutoka Newcastle United ambapo Newcastle wameendelea kusisitiza kuwa mshambuliaji huyo wa Kiswidi hayupo sokoni, Liverpool sasa inaonekana kuelekeza nguvu zake zaidi kwa Ekitike kama mbadala wa muda mrefu.
Katika hatua ya kuimarisha safu ya ushambuliaji, Liverpool si tu kwamba wanazungumza na Frankfurt kuhusu ada ya uhamisho wa Ekitike, bali pia mazungumzo yameanza upande wa mchezaji na mawakala wake, ambapo taarifa zinaeleza kuwa kuna maendeleo chanya katika pande zote mbili, klabu na mchezaji.