Karibia watu 300 wameuawa na RSF Kordofan Kaskazini

Nchini Sudan, wapiganaji wa RSF wameua karibu watu 300 kufuatia mashambulio katika jimbo la Kordofan Kaskazini yaliyoanza siku ya Jumamosi.

Kundi la haki za binadamu la Wanasheria wa Dharura, limesema wapiganaji wa RSF walishambulia vijiji kadhaa siku ya Jumamosi karibu na mji wa Bara, ambao wanamgambo hao wanadhibiti.

Katika kijiji kimoja, Shag Alnom, zaidi ya watu 200 waliuawa kwa kuchomwa moto ndani ya nyumba zao au kupigwa risasi.

Wanaharakati hao wameongeza kuwa, mashambulio katika vijiji vingine yalisababisha maafa ya raia 38, huku makumi ya wengine wakitoweka na hawajulikani waliko.

Siku iliyofuata, kundi hilo lilisema, RSF ilishambulia kijiji cha Hilat Hamid na kuua watu 46, wakiwemo akina mama wajawazito na watoto.

Zaidi ya watu 3,400 walilazimika kukimbia, kulingana na Umoja wa Mataifa.

RSF imekuwa ikipigana na jeshi la Sudan tangu Aprili 2023 katika vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo na kusababisha maafa ya maefu ya watu na mamilioni kusalia wakimbizi.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii