Idadi ya vifo yaongezeka Kenya

 IDADI ya raia waliofariki dunia kutokana na maandamano ya Jumatano imefikia 16, kwa mujibu wa taarifa ya shirika la Amnesty International.

Ripoti hiyo imeeleza kuwa  idadi ya watu waliopoteza  maisha imeongezeka kutoka wawili na kufikia 16 kutokana na majeraha ya risasi, huku wengine wakijeruhiwa vibaya wakati wa makabiliano kati ya waandamanaji na vikosi vya usalama.

Mkurugenzi wa Amnesty International nchini Kenya, Irungu Houghton, amesema idadi hiyo imethibitishwa na Tume ya Kitaifa ya Haki za Kibinadamu (KNCHR), na inatarajiwa kuongezeka kufuatia hali ya sintofahamu katika baadhi ya maeneo.

Maandamano hayo yaliyoongozwa na vijana, hasa wa kizazi kipya maarufu kama Gen Z, yalikuwa ni kumbukizi ya mwaka mmoja tangu maandamano ya awali dhidi ya muswada wa fedha yaliyogharimu maisha ya zaidi ya watu 60.

Vurugu hizo zimeripotiwa kuendelea kusambaa katika maeneo mbalimbali, huku mashirika ya haki za binadamu yakitoa wito wa uchunguzi wa haraka na uwajibikaji wa vyombo vya dola. 

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii