Waandamanaji 2 wa Gen Z Wapigwa Risasi na Polisi

Maandamano yanayoendelea ya kizazi cha Gen Z katikati mwa Jiji la (CBD) jijini Nairobi yameanza kuchukua mkondo mbaya. 

Maandamano hayo, yaliyokusudiwa kuwaenzi waliouawa wakati wa maandamano ya mwaka 2024, yamekuwa ya amani kwa kiasi kikubwa. Hata hivyo, waandamanaji wawili wamepigwa risasi na maafisa wa polisi wa kukabiliana na ghasia huku maandamano yakizidi kupamba moto katikati mwa jiji kuu.

Citizen TV ilishiriki video inayoonyesha waandamanaji wawili waliojeruhiwa wakikimbizwa katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta (KNH) kwa matibabu. Video hiyo ya kuhuzunisha ilimuonyesha mmoja wa wanaume akilia kwa maumivu wakati alipokuwa akipokelewa na timu ya matibabu KNH. 

Mwandamanaji aliyesaidia kuwapeleka majeruhi hospitalini alieleza kuwa kundi la maafisa wa polisi watano liliwazingira na kuanza kuwapiga. 

Alifichua kuwa mmoja wao amejeruhiwa vibaya baada ya kupigwa risasi kichwani. "Maafisa kama watano walikuja na kutuzingira kisha wakaanza kutupiga na kufyatua risasi kiholela. Katika hali hiyo, mtu mmoja alipigwa risasi karibu na shavu na amejeruhiwa vibaya sana," alisema mwandamanaji huyo.

Wakenya wamejitokeza kwenye mitandao ya kijamii kulaani kitendo cha polisi kuwapiga risasi waandamanaji.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii