Mama Adaiwa Kuwaua Watoto Wake Wawili Baada ya Kukorofishana na Mumewe

Wasichana wawili wadogo wanaripotiwa kufariki baada ya mama yao mwenye umri wa miaka 26, Mary Mushi, kudaiwa kuwachoma kisu tumboni. 

Baba mkwe wa Mary, Nicholas Kileka, alisimulia tukio hilo la kutisha, akieleza kuwa aliondoka nyumbani mapema asubuhi na kumpeleka mmoja wa wajukuu zake, Glory, ambaye wanaishi naye, kwa mama yake kabla ya kuelekea kazini. Wakati akiendelea na shughuli zake za kila siku, Nicholas alipokea simu saa saba mchana, akiarifiwa kuwa alihitajika kurudi nyumbani kwa haraka.

“Nilipofika nyumbani, nilikuta watu wanalia. Nilipoingia chumbani, nilikuta wajukuu wangu wakiwa wamefariki juu ya kitanda. Mkubwa wao, mwenye umri wa miaka minne, alikuwa amechomwa kisu mara mbili kifuani na tumboni, huku mdogo wake akiwa amechomwa mara moja tumboni,” alieleza.

Aliongeza kuwa mama yao pia alikuwa amelala kando ya watoto akiwa na majeraha matatu ya kisu. “Tulidhani wote wamekufa, lakini katikati ya vilio na taharuki, mtu mmoja aligundua kuwa Mary alikuwa bado hai.

Alipelekwa haraka katika hospitali ya karibu kupata huduma ya kwanza kabla ya kuhamishiwa hospitali nyingine kufanyiwa upasuaji,” Nicholas alisimulia. Babu huyo aliyejaa huzuni alisema kuwa Mary kwa sasa alikuwa nje ya hatari na anapata nafuu hospitalini.

Alisema mwanawe, ambaye ni baba wa watoto waliouawa, alipatwa na mshtuko mkubwa na kuonekana kupoteza mwelekeo. Nicholas aliongeza kuwa mwanawe aliweza tu kujibu salamu kabla ya kujitenga kimawazo kutokana na mshtuko na huzuni mkubwa.


Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii