Mgombea asiyekuwa na udhamini usiopungua watu watano kukosa sifa uchaguzi mkuu TFF

MWENYEKITI wa Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu (TFF), Kiomoni Kibamba amesema mgombea asiyekuwa na wadhamini zaidi ya watano hatapitishwa kugombea kwenye uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika Tanga, Agosti 16.

Wagombea 25 kati yao sita wakiwa ni wa nafasi ya urais na wengine wa ujumbe wa kamati ya utendaji wamerudisha fomu kuwania uchaguzi huo.

Akizungumza na waandishi wa habari, Kibamba alisema kama mgombea hana udhamini usiopungua wa watu watano anakosa sifa za kushiriki kwenye uchaguzi huo.

Kibamba alisema kazi yao ni kusimamia kanuni zilizotungwa na mkutano mkuu. Alisema kama udhamini una shida au hauna shida, kwenye kamati ya uchaguzi si mahala pa kupeleka malalamiko isipokuwa kwenye Mkutano Mkuu wa TFF.

Awali, wakirejesha fomu, wagombea wa urais, Ally Mayay, Shija Richard, Dk Mshindo Msolla na Mustapha Himba walilalamikia kukosa udhamini wakidai wajumbe wote wamemdhamini rais wa sasa wa TFF, Wallace Karia.

Kuhusu mapingamizi, Kibamba alisema wametupilia mbali pingamizi la Yanga dhidi ya Karia kwa sababu Mtendaji Mkuu wa klabu hiyo, Andre Mtine aliyewasilisha pingamizi hilo hakutokea, badala yake alimtuma wakili kinyume na kanuni za uchaguzi za TFF.

“Tunaendelea na usaili, mpaka sasa tumesaili 12 kati ya 25 na tunaendelea na usaili kesho, mapingamizi yaliwekwa lakini aliyeleta pingamizi aliitwa kwenye kamati lakini hakuja, kwa maana hiyo mapingamizi yalitupiliwa mbali kwa sababu kanuni ya 11 kanuni ndogo ya sita ya uchaguzi inasema aliyeleta pingamizi anatakiwa kuja mwenyewe kwenye usikilizwaji wa pingamizi hilo, Karia alikuja lakini Mtendaji Mkuu wa Yanga hakuja,” alisema Kibamba.

Wakati huo huo jopo la mawakili watano kutoka Kampuni ya Haki Kwanza Advocate limepeleka maombi Baraza la Michezo la Taifa (BMT) likitaka waingilie kati Uchaguzi Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).

Mawakili hao walisema wanaitaka BMT iangalie uchaguzi huo kuhakikisha unafuata sheria na kanuni sahihi hususani kwa nafasi ya urais.

Vilevile mwishoni mwa Juni, Yanga ilimuwekea pingamizi Karia wakiitaka kamati ya uchaguzi chini ya mwenyekiti wake, wakili Kilomoni Kibamba kumuondoa katika kinyang’anyiro cha uchaguzi huo wakiwa na hoja tatu.

Walitaja hoja hizo kuwa ni matumizi mabaya ya madaraka kwa mgombea mmoja kuchukua wadhamini 46 kati ya 47.

Wakizungumza Dar es Salaam jana, mawakili hao walisema wamewasilisha barua kuitaka BMT iingilie kati uchaguzi huo kwa sababu mgombea mmoja amechukua wadhamini wote na kueleza hiyo ni hila ya uchaguzi.

Wakili Juma Nassoro alisema wameingilia kati baada ya malalamiko mengi kujitokeza na kwamba wamefanya hivyo bila kutumwa na mgombea yeyote.

“Kama mnavyofahamu kanuni za uchaguzi zinataka mgombea wa urais wa TFF lazima apate wadhamini wasiopungua watano, huyo mgombea mmoja amechukua wadhamini 46 isipokuwa moja, ambayo sasa imebainika hiyo moja imetoka klabu ya Yanga,” alisema Nassoro na kusisitiza kama BMT haitachukua hatua watalipeleka suala hilo mahakamani.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii