MAMILIONI ya watu wanaokimbia mapigano nchini Sudan wanakabiliwa na hali mbaya ya njaa, huku wakisaka hifadhi katika mataifa jirani ambayo yenyewe tayari yanakumbwa na uhaba wa chakula.
Kwa mujibu wa Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP), wakimbizi zaidi ya milioni 4 wako hatarini zaidi kutokana na upungufu wa misaada katika nchi kama Jamhuri ya Afrika ya Kati, Misri, Ethiopia, Libya, Uganda na Chad.
Naye Mratibu wa Dharura wa WFP, Shaun Hughes, amesema kuwa licha ya wakimbizi hao kukimbia ili kuokoa maisha yao, bado wanakumbana na hali ya kukata tamaa, njaa na ukosefu wa rasilimali katika maeneo wanayokimbilia.
Sudan imekumbwa na mapigano makali kati ya jeshi la taifa na wanamgambo wa RSF, hali iliyopelekea vifo vya watu zaidi ya 40,000 na wengine takriban milioni 13 kuyakimbia makazi yao.
WFP imeonya kuwa hali ya kibinadamu inaendelea kuzorota kwa kasi, na imetoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuongeza msaada ili kuzuia janga kubwa la kibinadamu.