Idadi ya Vifo yaongezeka ajali ya Same hadi kufikia 39

Idadi ya watu waliofariki katika ajali ya magari mawili kugongana uso kwa uso Wilaya ya Same, mkoani Kilimanjaro imeongezeka na kufikia 39.

Ajali hiyo ilitokea Juni 28, 2025 katika eneo la Sabasaba, Same mjini ikihusisha basi la Kampuni ya Chanel One lililokuwa likitokea Moshi kwenda Tanga na basi dogo aina ya coaster lililokuwa likitokea Same mjini kwenda Moshi kugongana uso kwa uso na kuwaka moto wakati abiria wakiwa ndani ya magari hayo.

Akizungumza na Mwananchi leo Juni 30,2025 Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu amesema vifo kutokana na ajali hiyo vimeongezeka kutoka 38 vya awali na kufikia 39 baada ya mmoja wa majeruhi waliokuwa wanaendelea na matibabu kufariki dunia.

Akizungumzia hali za majeruhi, amesema mpaka sasa 22 kati ya 28 wameruhusiwa kutoka hospitalini baada ya afya zao kuimarisha.

Amesema vipimo vya vinasaba (DNA) vya miili 33 vimeshapelekwa Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali ili kuitambua na kuikabidhi kwa familia kwa ajili ya taratibu za mazishi.

Mabaki ya miili iliyotambuliwa mpaka sasa ni mitano huku mingine 33 ikifanyika vipimo hivyo kutokana na kuharibika.


Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii