KADA wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Emmanuel Mkuchu, amekamilisha hatua ya awali ya kugombea nafasi ya udiwani kwa kurejesha fomu ya kuwania nafasi hiyo katika Kata ya Kunduchi, jijini Dar es Salaam.
Mkuchu alichukua fomu hiyo ya kugombea udiwani jana, Juni 29, 2025, katika ofisi za CCM za kata hiyo, kama sehemu ya mchakato wa uteuzi wa wagombea ndani ya chama hicho tawala.
Leo, tarehe 30 Juni 2025, Mkuchu amerudisha rasmi fomu hiyo, hatua inayoashiria dhamira yake ya kuwatumikia wananchi wa Kunduchi kupitia nafasi ya udiwani endapo atapitishwa na chama chake na kushinda uchaguzi.
Akizungumza mara baada ya kurejesha fomu, Mkuchu amewashukuru wanachama wa CCM na wakazi wa Kunduchi kwa ushirikiano, huku akieleza kuwa ana nia thabiti ya kuleta maendeleo kwa kushirikiana na wananchi endapo atapewa ridhaa ya kuwa diwani.