Kampuni ya Rasilimali ya Madini Sudan (SMRC) imethibitisha kuwa wachimbaji 11 wa dhahabu wamefariki dunia baada ya kuangukiwa na mgodi katika eneo la Kirsh al-Fil, jangwa la Howeid, kati ya miji ya Atbara na Haiya linalodhibitiwa na jeshi.
Kwa mujibu wa taarifa ya kampuni hiyo, wachimbaji wengine saba walinusurika lakini walijeruhiwa na kukimbizwa hospitalini kwa matibabu. Hata hivyo, haijafahamika ni lini ajali hiyo ilitokea.
SMRC ilieleza kuwa mgodi huo ulikuwa umesitishwa awali kutokana na hofu ya usalama wa wachimbaji, lakini haikubainisha ni kwa vipi shughuli ziliendelea hadi tukio hilo kutokea.