BAADA ya siku tano za hekaheka ndani ya Tamasha la Kimataifa la Filamu Zanzibar (ZIFF), msimu wa 28, tamasha hilo litafungwa rasmi kesho huku washindi mbalimbali wa filamu wakaitarajiwa kutangazwa.
Jopo la majaji, lililokuwa likifanya kazi kwa bidii kutathmini kazi zote zilizowasilishwa, limemaliza kazi yake na linatarajiwa kutangaza washindi kesho. Tuzo mbalimbali zenye heshima kubwa zitatolewa katika tamasha hilo.
Licha ya tuzo hizo muziki wa taarabu ambao ni kiini cha Utamaduni wa Visiwa vya Zanzibar unatarajiwa kutoa burudani maalumu ya kufunga shamrashamra hizi kwa mwaka 2025.
Kauli hiyo imetolewa na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Tamasha hilo, Joseph Mwale wakati akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za tamasha hilo zilizopo katika Jengo la Sinema la zamani la Majestic, barabara ya Vuga mjini Unguja, visiwani Zanzibar.
Mwale, ameelezea kuridhishwa kwake na mafanikio makubwa ya tamasha hili, akisisitiza umuhimu wa ZIFF katika kuendeleza hadithi za Kiafrika na kuunganisha tamaduni mbalimbali kupitia sanaa ya filamu akidai mafanikio hayo yanathibitisha nafasi ya Zanzibar kama kitovu muhimu cha filamu na utamaduni katika ukanda wa Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla.
Mwale amemtaja mgeni rasmi katika hafla hiyo ya kilele atakuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi, Hamza Hassan Juma.
Kufikia tamati kwa ZIFF msimu wa 28 kunaashiria kukamilika kwa programu nzima iliyoshuhudia uonyeshaji wa filamu zaidi ya 70 zilizokuwa zikishindana, kutoka nchi zaidi ya 100 duniani kote.
Mbali na uonyeshaji wa filamu, tamasha hili limekuwa jukwaa la kipekee la kuendesha programu mbalimbali, ikiwemo programu maalum za wanawake wakifunzwa ujasiriamali na watoto waliofunzwa utengenezaji wa vikaragosi.
Pia, warsha na ‘master class’ zikijumuisha mafunzo muhimu kama vile uandishi wa ‘subtitle’ na utengenezaji wa filamu fupi na ndefu zikilenga kukuza vipaji na ujuzi katika tasnia ya filamu barani Afrika na duniani kote.