LADY JAY DEE AZINDUA RASMI KITABU CHAKE “DIARY YA LADY JAY DEE” BAADA YA MIAKA 25 YA SAFARI YA MUZIKI

Mwanamuziki mkongwe na msanii wa kike wa kwanza kung’ara kwenye Bongo Fleva, Judith Wambura Mbibo, maarufu kama Lady Jay Dee, jana alizindua rasmi kitabu chake kipya kinachoitwa “Diary ya Lady Jay Dee”, akitimiza miaka 25 ya safari yake ya muziki iliyojawa na mafanikio, changamoto, na ushindi wa kweli wa mwanamke katika sanaa.

Katika tukio lililofanyika jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na wageni waalikwa mbalimbali wakiwemo wasanii, wanahabari, mashabiki na wadau wa sanaa, Lady Jay Dee alionekana mwenye furaha kubwa huku akishukuru Mungu kwa kumuwezesha kufikia hatua hiyo muhimu ya maisha. Alitia saini nakala ya kwanza ya kitabu hicho mbele ya hadhira, akisema kuwa hiyo ni ndoto aliyokuwa nayo kwa muda mrefu.


kupitia ukurasa wake wa instagram ameandika "Dear God I thank you finally am signing books". 

Kitabu cha “Diary ya Lady Jay Dee” kinachukua wasomaji katika safari ya maisha ya msanii huyo, kuanzia alipoanza muziki mapema miaka ya 2000, hadi alipo leo – akiwa ni mmoja wa wanamuziki wa Tanzania waliodumu kwa muda mrefu na kuacha alama ya kudumu kwenye tasnia ya muziki barani Afrika.


Ndani ya kurasa za kitabu hicho, Lady Jay Dee anazungumzia kwa uwazi masuala ya maisha yake binafsi, changamoto katika ndoa na mahusiano, vita dhidi ya magonjwa, mafanikio yake kitaaluma, pamoja na misimamo yake kuhusu nafasi ya mwanamke kwenye jamii na muziki.

Tukio la jana limepokelewa kwa hisia kali mitandaoni, ambapo mashabiki wake wengi walimpongeza kwa ujasiri wa kufungua moyo wake na kuweka historia hiyo kwenye maandishi.

 

 

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii