Msanii nyota wa muziki wa Bongo Fleva, Mbosso, ameachia rasmi Extended Playlist (EP) yake mpya iitwayo “Room Number 3”, ambayo imezua msisimko mkubwa miongoni mwa mashabiki wake. Hii ni kazi yake ya kwanza kubwa kuachia tangu kutengana na lebo ya WCB Wasafi, hatua ambayo ilishangaza wengi lakini pia ilionyesha dhamira yake ya kusimama pekee kama msanii huru.
Kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii, Mbosso amewaomba mashabiki wake kuendelea kumpa sapoti, akisisitiza kuwa muziki wake bado unazungumza kwa niaba ya mioyo ya watu, japo safari hii anatoka bila kivuli cha lebo kubwa nyuma yake.
“Room Number 3 siyo tu EP, ni hadithi ya maisha yangu, mapenzi, maumivu na matumaini,” aliandika Mbosso kwenye Instagram. “Ni kazi niliyoweka moyo wangu wote. Naomba sapoti yenu kama mwanzo mpya katika safari yangu ya muziki.”
EP hiyo ina nyimbo 6 pamoja na wimbo mmoja wa nyongeza, na tayari mashabiki wameanza kusifia ubora wa uandishi, uimbaji na hisia zilizopo ndani ya kazi hiyo.
Kutengana kwa Mbosso na WCB hakujakuwa kikwazo, bali ni nafasi mpya kwake kujitambulisha upya na kuonesha uwezo wake nje ya mfumo wa lebo. Mashabiki wake wanaamini kuwa bado ana nafasi kubwa ya kung’ara zaidi akiwa kama msanii huru.