Msanii maarufu wa muziki wa Bongo Fleva, Bilnass, amefungua ukurasa mpya wa majadiliano kwenye tasnia ya muziki kwa kutoa waraka mzito kupitia ukurasa wake wa Instagram, akielezea kwa kina namna alivyodhulumiwa na wadau mbalimbali katika sekta ya sanaa, hasa upande wa usambazaji wa kazi zake.
Katika andiko lake, Bilnass anasema:
“Juzi niliandika Waraka kuhusu vitu vingi vilivyomo kwenye upande wa pili wa Tasnia na Sanaa Zetu. Lengo sio kuwavunja moyo au kuwatisha watu wapya au vijana wenye ndoto ya kuingia kwenye tasnia, bali ni kuwakumbusha na kuwaandaa kukabiliana na ulimwengu wa kweli.”
Msanii huyo aliyejizolea umaarufu kupitia nyimbo kama “Puuh”, amefichua kuwa licha ya kazi hiyo kuwa na mafanikio makubwa, hajawahi kulipwa hata senti moja kutoka kwenye mauzo ya kidigitali ya wimbo huo. Bilnass anadai kuwa licha ya kuwepo kwa mikataba ya kisheria, bado analazimika “kuomba au kubembeleza” ili kupata haki yake.
“Kuna dhulma nyingi zinafanywa na wadau, labels, managers, promoters, wamiliki wa media, distribution company n.k. Lakini leo wacha nianze na upande wa distribution, na nitamuelezea Michael Mlingwa A.K.A Mx Carter kama mmoja wa wadau muhimu lakini wadidimizaji wakubwa kwenye maswala ya uuzaji na usambazaji wa kazi zetu.”
Kwa mujibu wa Bilnass, Mx Carter na washirika wake wamekuwa wakinufaika na kazi za wasanii bila kuwapa malipo stahiki, hali ambayo imeathiri si tu kipato cha wasanii bali pia morali na maendeleo ya muziki nchini.
“Mimi ni mmoja wa wahanga wa dhulma hiyo, na naamini baada ya hili mtasikia vilio vingi vyenye kufanana na hiki,” aliongeza.
Andiko hili limetikisa mitandao ya kijamii na kuchochea mijadala mikali kuhusu usalama wa haki za wasanii ndani ya mfumo wa usambazaji na mapato ya muziki wa kidigitali. Wengi wamepongeza ujasiri wa Bilnass kuzungumza wazi, huku wakitaka hatua madhubuti zichukuliwe kulinda wasanii wengine dhidi ya dhulma kama hiyo.
Bilnass ameahidi kuwa huu ni mwanzo tu, na ataendelea kufichua zaidi kuhusu changamoto na vitendo vya dhulma vinavyoendelea kufanyika nyuma ya pazia la tasnia ya burudani.
“Nitawasimulia mengi yanayofanywa na watu kama Mx Carter na washirika wao,” alihitimisha.