RAPA SILENTÓ AHUKUMIWA KIFUNGO CHA MIAKA 30 JELA

Rapa maarufu kutoka Atlanta, Silentó, anayejulikana sana kwa kibao chake kilichotamba mwaka 2015 Watch Me (Whip/Nae Nae),” amehukumiwa kifungo cha miaka 30 jela baada ya kukiri kosa la kumuua binamu yake kwa kumpiga risasi mwaka 2021.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Jumatano na Mwanasheria wa Wilaya ya DeKalb, rapa huyo mwenye umri wa miaka 27, ambaye jina lake halisi ni Ricky Lamar Hawk, alikiri kosa la kuua bila kukusudia na shambulio lililosababisha kifo cha binamu yake, Frederick Rooks III.

Tukio hilo liliripotiwa na Polisi wa Kaunti ya DeKalb, ambao walimpata Rooks akiwa amejeruhiwa vibaya kwa risasi, huku maganda ya risasi yakikutwa katika eneo la tukio. Uchunguzi wa picha za usalama ulibaini Silentó akikimbia eneo hilo kwa kutumia gari jeupe aina ya BMW.

Baadaye, wachunguzi walifanikiwa kulinganisha maganda ya risasi yaliyopatikana eneo la tukio na bunduki iliyogunduliwa kuwa inamilikiwa na Silentó. Siku 10 baada ya tukio hilo, alikiri kuhusika na mauaji hayo, akieleza kwamba alihusika moja kwa moja, ingawa alidai kuwa alikuwa akipambana na matatizo ya afya ya akili tangu utotoni.

Inadaiwa kuwa mwaka 2020, Silentó alijaribu hata kujiua kutokana na msongo mkubwa wa akili. Licha ya kutolewa kwa hoja hizo mahakamani kama sehemu ya utetezi, hakimu aliamua kuwa kifungo cha miaka 30 ni adhabu inayostahili kutokana na uzito wa kosa hilo.

Hukumu hiyo imeleta hisia tofauti miongoni mwa mashabiki na wanajamii, wengi wakieleza masikitiko yao juu ya kuporomoka kwa nyota wa muziki aliyewahi kung’ara kimataifa, huku wengine wakisisitiza umuhimu wa kushughulikia matatizo ya afya ya akili mapema.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii