Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imemhukumu Ofisa Habari na Mawasiliano wa Klabu ya KenGold Joseph Mkoko(34) kulipa faini ya Sh1 milioni au kwenda jela miaka miwili baada ya kupatikana na hatia ya kuomba na kupokea rushwa.
Mkoko anadaiwa kuomba rushwa ya Sh1.5 milioni kutoka kwa mchezaji wa zamani wa timu ya mpira wa miguu ya Vital’O ya Burundi ili amsaidie kusajiliwa na timu yake ya KenGold na kupata upendeleo wa kupangwa kwenye kikosi cha kwanza cha timu hiyo.
Katika kesi ya msingi mshtakiwa anakabiliwa na kesi ya jinai namba 13138 ya mwaka 2025 yenye mashtaka mawili ya kuomba na kupokea rushwa.
Ambapo afisa habari huyo anadaiwa kutenda makosa yake kati ya Disemba Mosi 2024 hadi Disemba 31, 2024 eneo la Kibaha mkoani Pwani.
Katika shtaka la kwanza mshitakiwa anadaiwa kuomba rushwa ya Sh1.5milioni na shtaka pili anadaiwa kupokea kiasi hicho cha rushwa kutoka kwa mchezaji mmoja wa zamani wa timu ya mpira wa miguu ya Vital’o ya Burundi ili amsaidie kusajiliwa katika timu yake.
Ikiwa anadaiwa kuwa kutenda makosa hayo ni kinyume na kifungu cha 15(1)(a) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Sura ya 329 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2024.
Kwa mara ya kwanza Mkoko alifikishwa mahakamani hapo Mei 30, 2025 na kusomewa mashtaka hayo hata hivyo alikuwa nje kwa dhamana.
Baada ya kutiwa hatiani mshtakiwa amekiri mashtaka yake wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kusomewa hoja za awali ambapo kabla ya kusomewa hoja za awali, alikumbushwa mashtaka yake kwa kusomewa upya na ndipo alipokiri mashtaka yake na mahakama hiyo kumtia hatiani.
Hukumu hiyo imetolewa Juni 11, 2025 na Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Beda Nyaki baada ya mshtakiwa huyo kukiri mashtaka yake.
Hata hivyo mshtakiwa huyo amefanikiwa kulipa faini hiyo na hivyo kukwepa kifungo cha miaka miwili jela.
Ili kupata taarifa zaidi endelea kutufuatilia kupitia website yetu ya www.jembenijembe.com kupitia Instagram ,Facebook, tikok,x zamani twitter pamoja na YouTube